Burudani

Nyangamalle wa TAFCA ajiuzulu wadhifa wake

DAR ES SALAAM:RAIS wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Adrian Nyangamalle, amejiuzulu nafasi yake.

Taarifa za kujiuzulu kwake zimetolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Nyangamalle amesema ametafakari kwa kina na kuchukua hatua hiyo kwa maslahi mapana ya maendeleo ya tasnia na sekta ya sanaa kwa ujumla, huku akiahidi kuendelea kutoa mchango wake kama msanii na mdau mzoefu katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk. Kedmon Mapana, amepokea rasmi barua ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo.

Nyangamalle ameishukuru serikali, BASATA na wadau wengine kwa kumpa ushirikiano chanya muda wote alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama rais wa shirikisho hilo.

Pia, amevishukuru vyama, wanachama na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAFCA kwa kumuamini na kumpa heshima ya kuwa rais wa kwanza wa shirikisho hilo.

Dk. Mapana amepongeza hatua hiyo, akisema kuwa ni uamuzi wa busara unaoonesha ukomavu wa kiuongozi na kujali maslahi mapana ya sekta ya sanaa.

Ameahidi kuwa BASATA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha maendeleo ya sanaa na wasanii nchini yanaimarika.

Hatua hii imepokelewa kwa mtazamo chanya, huku wadau wa sanaa wakitarajia mwelekeo mpya wa shirikisho hilo katika kukuza ubunifu na ustawi wa wasanii wa Tanzania.

Related Articles

Back to top button