Nikole Kidman, mumewe kuhama Marekani
LAS VEGAS: MUIGIZAJI Nicole Kidman amesema yupo katika fikra za kuhama Marekani huko Hollywood kwa sababu zake binafsi na si za kisiasa.
Mshindi huyo wa tuzo ya Oscar na mumewe, mwimbaji Keith Urban, wanafikiria kuhama kwa pamoja kutoka Marekani hadi nchi yao ya Australia kufuatia kile kilichotajwa kuwa “Mwaka wao mbaya zaidi kuwahi kutokea.”
Mwaka umekuwa mgumu sana kwa wanandoa hao, huku Nicole, akihuzunika kumpoteza mama yake, Janelle, ambaye aliaga dunia mwezi Septemba akiwa na umri wa miaka 84.
Habari za kupoteza zilikuja kabla tu mwigizaji huyo kupokea tuzo ya Mwigizaji Bora wa Filamu katika Tamasha la Filamu la Venice kupitia filamu ya ‘Babygirl’.
Vyanzo vya karibu vya wanandoa hao vimedai kwamba ratiba ya Nicole imeongeza shida kwa kipindi chote walichoishi Marekani ambapo kwa mwaka uliopita, amekuwa akisafiri mno kutokana na ahadi mbalimbali zinazohusiana na filamu zake zikiwemo ‘Babygirl’ na tamthilia ya uhalifu ‘Scarpetta’.
Vyanzo hivyo vimeeleza zaidia kwamba mwigizaji huyo pia ametumia muda mfupi sana na mumewe katika mwaka uliopita, kutokana na ratiba zake kumbana. “Wasiwasi mkubwa kwenye akili za kila mtu ni kiasi gani anaweza kuchukua muda wa mapumziko ili kuwa karibu na mwenzi wake lakini kwa sasa amekuwa na ratiba ngumu mno.”
Keith, ambaye pia ana umri wa miaka 57, naye anafikiria kuacha kazi yake ya muziki ili kumuunga mkono mkewe Nicole. Kufuatia kuishi kwake Las Vegas kwa miaka mingi.
Kuhama kwa familia hiyo kurudi Australia kutamruhusu Nicole kuungana tena na mizizi yake na kupata faraja kutokana na kutingwa na ratiba ndefu na ngumu.
Wiki kadhaa zilizopita, nyota wa Hollywood, Ellen DeGeneres na Eva Longoria walikuwa kwenye habari kufuatia uamuzi wao wa kuondoka Marekani kabla ya urais wa Donald Trump.