Ligi Kuu

Ngassa, Fikiri Elias wajizolea tuzo za Septemba

DAR ES SALAAM: KOCHA MKuu wa Coastal Union, Fikiri Elias ameibuka Kocha Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu Bara huku kiungo wa Dodoma Jiji, Berno Ngassa akitajwa kuwa mchezaji bora wa mwezi huo.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi leo Jumatano imefafanua Fikiri ameibuka kidedea akiwabwaga Steve Barker wa Simba SC na Vicent Mashami wa Dodoma Jiji.

Katika mwezi huo, Fikiri aliiongoza Coastal ya Tanga kushinda michezo yote miwili na kupanda kutoka nafasi ya 15 hadi ya 11 kwenye msimamo wa ligi.

Naye Ngassa alionesha kiwango kizuri na kuwashinda Maabad Maabad wa Coastal na Anuary Jabir wa Polisi Tanzania, alioingia nao fainali katika mchakato huo uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Ngassa alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo miwili waliyoshinda bao 1-0 kwenye kila mchezo.

Mechi dhidi ya Mashujaa alifunga bao na mechi yao ya mwisho dhidi ya Namungo alitoa pasi ya bao pekee lililofungwa na Yassin Mgaza.

Kamati pia imeteua mabao matatu ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata bao bora la mwezi Septemba. Mabao hayo ni Haroun Lyawatwa (Mashujaa v Singida BS), Anuary Jabir (Polisi V Mbeya City) na Mohamed Damaro (Singida BS v Namungo).

Pia, Ramadhan Kalanje wa KMC amchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Septemba wa Ligi ya Championship, akiwashinda Abiud Mtambuku wa Mbeya Kwanza na kipa Haroun Mandanda wa Rhino Rangers.

Kocha wa KMC, Mohamed Muya amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo, aliyeiongoza timu yake kushinda michezo yote mitatu iliyocheza akiwashinda Salvatory Edward wa Rhino Rangers na Said Lyakuka wa Transit Camp.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button