Neema yatua timu ya Taifa ya Raga

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya utengenezaji wa vifaa vya michezo kutoka nchini Ufaransa ya Sergio mat imekabidhi rasmi vifaa vya michezo kwa timu ya taifa ya mchezo wa raga nchini.
Tukio hilo limefanyika baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya Chama cha mchezo wa raga nchini na kampuni hiyo ya utengenezaji vifaa vya michezo kutoka nchini Ufaransa.
Tukio hilo liliongozwa na uwakilishi na Ofisa wa Michezo kutoka Baraza la michezo la Taifa BMT, Charles Maguzu ambapo ameishukuru kampuni kwa msaada wa vifaa ambavyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa timu ya taifa ya raga ya wanawake.
Amewapongeza viongozi wa chama cha mchezo wa raga nchini kwa kuonesha kwa vitendo dhana ya mashirikiano ya kimataifa katika kuendeleza michezo, jambo hilo lisingiwezekana bila wao kuwa na mahusiano mazuri na kampuni hiyo kutoka nchini Ufaransa.
“Kwa niaba ya BMT, tutashirikiana na viongozi wa mchezo husika kuhakikisha kuwa vifaa hivi vinawafikia walengwa na kutumika kadri inavyotakiwa kwa kuandaa timu ya Taifa ya Wanawake,” amesema Maguzu.
Naye Mkuu wa maendeleo ya wanawake katika mchezo wa raga nchini, Fatma el kindiy amesema kupitia vifaa hivyo itafungua milango kwa wachezaji wa mchezo huo kuzidi kujitangaza katika soko la kimataifa kimichezo hususani kwa wanawake.