Nandy aibuka mshindi kesi dhidi ya Tongenyama

DAR ES SALAAM: MSANII Faustina Charles ‘Nandy’ ameibuka mshindi katika kesi iliyofunguliwa dhidi yake na msanii mwenzake Mozee Kamana, maarufu kama Mr. Tongenyama, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali madai yaliyowasilishwa dhidi yake.
Kesi hiyo iliyofunguliwa tangu Julai mwaka jana ilihusu madai ya Tongenyama kwamba Nandy alitumia wazo au ubunifu unaohusishwa na jina ‘Tonge Nyama’ katika kazi yake bila ruhusa.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama Kuu imeona madai hayo hayana msingi na hivyo Nandy kuibuka mshindi.
Akizungumza Dar es Salaam leo baada ya hukumu hiyo, Nandy amesema anashukuru mahakama kwa kutenda haki, akisema mchakato wa kufuatilia kesi hiyo haukuwa rahisi kutokana na muda na gharama zilizohitajika.
Amesema kwake jambo kubwa ni kuona haki imetendeka na hatimaye ameweza kushinda kesi hiyo iliyokuwa ikiendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Namshukuru Mungu na nashukuru Mahakama Kuu kwa kutenda haki. Kesi hii ilianza tangu Julai mwaka jana na leo hukumu imetoka, nimeibuka mshindi,” amesema Nandy, akisisitiza kuwa amefurahishwa na uamuzi huo baada ya kupitia mchakato mrefu wa kisheria.
Kwa upande wake, mwanasheria wa Nandy, Clavery Mlowe wa Cosmic Attorneys, amesema Mahakama baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na pande zote haikubaini msingi wa madai kwamba Nandy alichukua kazi ya sanaa au ubunifu wa mtu mwingine.
Mlowe amesema upande wa Tongenyama pia uliwasilisha madai ya fidia kutokana na hasara uliodai kusababishwa, lakini mahakama haikuona msingi wa madai hayo.
Mlowe amesisitiza kuwa mtu anayehisi haki yake imekiukwa katika masuala ya kazi au biashara anapaswa kutumia utaratibu wa kisheria badala ya kuchukua hatua nyingine, akisema Mahakama ndiyo chombo chenye mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu migogoro hiyo.




