Mwili upo Mashujaa, roho ipo kwingine.

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Mashujaa FC, Chrispin Ngushi amesema bado matumaini yake ni kuendelea kuonyesha kiwango bora na kuweza kurejea kwenye klabu kubwa ikiwemo Yanga na kucheza soka la kulipwa nje.
Ngushi aliwahi kucheza Yanga kabla ya kupelekwa kwa mkopo Coastal Union msimu uliopita na sasa anaitumikia Mashujaa FC baada ya mkataba wake na Yanga kutamatika na kupewa ‘THANK YOU’.
Akizungumza na Spotileo, Ngushi amesema kuna maisha tofauti alipotoka kwenye timu hizo mbili na sasa alipokuwa, ana imani kila sehemu kuna mazingira ya kuishi.
Amesema mipango aliyokuwa nayo sio kuendelea kucheza Mashujaa FC, bali anahitaji kupambana zaidi kwa kuonyesha kiwango kizuri kwa ajili ya kuzishawishi timu kubwa kumsajili ikiwemo Yanga au Simba.
“Ni kweli nimepita Yanga na sasa niko Mashujaa, haina maana kuwa sitaweza kurudi kwenye timu kubwa bali ni jinsi ya kupambana uwanjani. Malengo yangu ni kuona ninarejea kucheza katika klabu kubwa au kucheza soka nje ya Tanzania,” amesema Ngushi.