Musiala afunguka afya yake

MUNICH: NYOTA wa Bayern Munich, Jamal Musiala, amewatoa hofu mashabiki waliokuwa na wasiwasi baada ya kupata changamoto katika michezo ya hivi karibuni.
Kauli yake imekuja baada ya kusambaa kwa video inayomuonesha akianguka uwanjani na kusaidiwa haraka na wachezaji wenzake.
Musiala ameandika ujumbe kwenye mtandao wake amesema amegundulika kuwa na hali ya kupoteza fahamu kwa muda mfupi na mara chache, inayosababishwa na changamoto katika mfumo wa neva, akisisitiza kuwa hali hiyo inatibika na kwa sasa haijaweka afya yake katika hatari.
Kupitia ujumbe wake kwa mashabiki, Musiala amesema amekuwa akipokea jumbe nyingi za watu waliokuwa na wasiwasi kuhusu afya yake, hivyo akaona ni muhimu kutoa ufafanuzi kuhusu hali anayopitia.
Amesema matukio hayo yanaweza kusababisha vipindi vifupi vya kupoteza fahamu, ikiwemo vilivyoonekana katika mchezo dhidi ya Leipzig pamoja na tukio la hivi karibuni dhidi ya Heidenheim.
“Nimegundulika kuwa na hali ya kupoteza fahamu kwa muda mfupi na mara chache, lakini inayotibika vizuri, inayosababishwa na changamoto katika mfumo wa neva,” amesema Musiala.
Kiungo huyo amesema kwa sasa yupo chini ya uangalizi na matibabu ya wataalamu, huku akiwa na matumaini makubwa ya kuendelea vizuri.
Musiala pia amesema Bayern Munich pamoja na watu wake wa karibu wamekuwa wakimpa msaada katika kipindi hiki, huku akisisitiza kuwa kwa mujibu wa wataalamu anaweza kuendelea na maisha yake ya kawaida na kufanya kile anachokipenda zaidi, ambacho ni kucheza soka.
Musiala amesema kwa sasa anajisikia vizuri na anaamini yupo kwenye njia sahihi ya kuimarika, huku akitaja kuendelea kupigania ushindi na mataji akiwa na timu yake pamoja na sapoti ya mashabiki kuwa miongoni mwa vitu vinavyomsaidia zaidi.
Hata hivyo, nyota huyo amewaomba mashabiki kuheshimu uamuzi wake wa kutoweka wazi zaidi kuhusu suala hilo, akisema anataka kulihifadhi ndani ya mduara wa marafiki zake wa karibu, klabu na wataalamu wanaomhudumia.




