Msama awaomba waimbaji wa injili kutoshikamana na Bongo Fleva

Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, amewaonya waimbaji wa nyimbo za Injili nchini Tanzania kuacha kushiriki majukwaa pamoja na wasanii wa Bongo Fleva, akisema kufanya hivyo ni kushiriki katika kumtukuza shetani.
Akizungumza na Spotileo jijini Dar es Salaam, Msama, ambaye pia ni muandaaji wa matamasha ya Injili, amesema waimbaji wa nyimbo za Injili wanapaswa kujitenga na majukwaa hayo kwa sababu uimbaji na uchezaji wa muziki wa Bongo Fleva hauhusiani na kumtukuza Mungu.
Pia amewatahadharisha wasanii wa Injili dhidi ya tamaa ya pesa, akisema kuna baadhi yao wanaoshiriki majukwaa yasiyo ya kiroho kwa sababu ya fedha, jambo linaloweza kuwapotosha na kuwatoa katika wito wao wa kumtumikia Mungu.
“Nawaonya waache kushiriki madhabahu za shetani. 2 Wakorinto 6:14-18 inasema: ‘Msiambatane pamoja na watu wasioamini.’ Pia, wajihadhari na kupenda pesa kupita kiasi, kwani pesa nyingine ni za maagano ya kuzimu,” amesema Msama.
Msama, ambaye ni mdau mkubwa wa muziki wa Injili, hivi karibuni alipokea tuzo ya heshima kama muandaaji bora wa matamasha ya Injili nchini Tanzania, yakiwemo Tamasha la Pasaka na Tamasha la Christmas.