Africa

Mpanzu kuanza na waarabu!

TUNISIA: WINGA wa Simba, Elie Mpanzu sasa  yupo huru kucheza michuano ya kombe la Shirikisho Afrika baada ya usajili wake wake kimataifa kukamilika na kupata leseni ya kushiriki michuano hiyo.

Mpanzu ni miongoni mwa usajili uliofanywa kipindi cha dirisha dogo na kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara na juzi Simba wamefanikiwa kupata kibali cha kumtumia katika michezo wa Kombe la Shirikisho Afrika na ataanza kazi dhidi ya CS Sfaxien siku ya Jumapili.

Akizungumza na Spotileo leo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema wakati watu wakisheherekea mwaka mpya wa 2025 wao walifanya kazi ya kupitisha usajili wa Mpanzu kimataifa.

“Tumefanikiwa kukamilisha usajili na kupata kibali cha Mpanzu kumtumia kwenye michuano ya kimataifa na atakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mechi yetu dhidi ya CS Sfaxien, “amesema.

Kuhusu maandalizi ya mchezo huo, Ahmed amesema kila kitu kimeenda vizuri na hali ya hewa sio mbaya sana kama ilivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya CS Constantine.

“Kazi iliyopo kwa sasa ni benchi la ufundi na wachezaji kufanya majukumu yao, hali ya hewa sio baridi sana maana kuna muda inakuja hali ya Mbeya, sio baridi kama ilivyo kwa CS Constantine ile ilikuwa hatari.

“Niwaondoe wanasimba hofu tumepokelewa vizuri sana ukizingatia ile hali ya mchezo uliopita kila mtu alikuwa akihofia tutafanyiwa figisu tukifika huku,” amesema.

 

 

Related Articles

Back to top button