Mahusiano

Mchekeshaji na Mc Kenya asimulia chanzo cha ndoa yake kuvunjika

NAIROBI: MCHEKESHAJI maarufu wa Kenya na muongozaji wa kipindi cha mahusiano cha Hello Mr. Right, Dr. Ofweneke, ameweka wazi kushangazwa na kuvunjika kwa ndoa yake ya pili na Christine Tenderess akidai alijitahidi kufanya kila kitu sawa lakini bado ndoa yake ilivunjika.

Hivi karibuni alivyohojiwa na channel moja ya mtandaoni akihojiwa na Willis Raburu baba huyo wa watoto watatu alisema aliweka maombi maalumu ya kuzungumza na Mungu kupitia sala akihoji kwa nini ndoa hiyo imevunjika wakati amejitahidi kuwa baba bora na anayejituma mno.

“Nilimwambia Mungu, nimejaribu kufanya kila kitu sawa. Nilikuwa msaidizi kwenye maombi na mwenye bidii kama baba watoto na hata kwa mke wangu, nilihakikisha kila kitu kiko sawa. Lakini bado hii ndoa imevunjika. Vipi naweza kusimama mbele ya watu kama Dr. Ofweneke na kuzungumza na wanaume waliopo kwenye ndoa?” alieleza.

 

Baada ya kutengana, alichukua muda kuchunguza mifumo ambayo inaweza kuwa imechangia mahusiano yake kushindwa. Akafananisha na namna alivyotengwa tangu utoto wake, akifichua kwamba mama yake alimwacha akiwa na umri wa wiki moja na baba yake alioa mke mwingine akiwa na umri wa miaka minne tu.

Alisema muda mwingi alikuwa akilelewa na watu mbalimbali huku akifanya kazi katika mashamba huko Magharibi mwa Kenya na Malava, hakuwahi kuku ana baba yake wala mama yake wa kambo hivyo anaamini huenda hali hiyo imesababisha pia ndoa yake kutodumu.

“Nilijitambua kuwa mimi ni mwanaume ambaye nikikupenda nakupa asilimia 100. Lakini wakati mwingine huwa sijitoi kwa sababu naogopa kwamba nikikupenda sana utaniacha, ikiwa mama yangu aliondoka basi na wewe unaweza kufanya hivyo, lakini pia huenda matumizi ya pombe nayo yamesababisha ndoa yangu kuvunjika,” alieleza Dr. Ofweneke.

Licha ya hofu hizi, Dr. Ofweneke alisema katika mahusiano yake ya sasa na Maryanne Baraza ataongeza upendo zaidi kwa kuwa mwanamke huyo amekuwa muwazi mno kwake na atapunguza matumizi ya pombe.

Hali ya uhusiano wa Ofweneke ilivutia umma mnamo Julai 7, 2024, alipomtambulisha Maryanne kama mpenzi wake kwenye kipichi cha Televisheni cha ‘Mr. Right’, ikiashiria ukurasa mpya katika maisha yake ya kimahusiano ambayo yaliwashangaza mashabiki wake.

Awali Ofweneke alioana na mwimbaji wa nyimbo za Injili, Nicah the Queen, ambaye walitengana naye mwaka wa 2016 kwa sasa wanaendelea kulea watoto wao wawili.

Related Articles

Back to top button