Burudani

Rapa Diddy akumbana na kesi mpya ya unyanyasaji wa kijinsia

NEW YORK: Marekani RAPA na mfanyabiashara maarufu Sean Combs maarufu P-Diddy, ambaye ni mmoja wa wasanii wa muziki wa rap waliofanikiwa zaidi, anakabiliwa na kesi nyingine ya unyanyasaji wa kijinsia baada ya mwanamke mwingine kujitokeza na tuhuma mpya dhidi yake.

P-Diddy, amekana madai yote ya unyanyasaji wa kijinsia na unyanyasaji wa kimwili, ikiwa ni pamoja na tuhuma za hivi karibuni dhidi yake.

Nyota huyo sasa anaripotiwa kuchunguzwa na shirikisho la uhalifu, ingawa hakuna dalili ya kuwepo kwa mashtaka yoyote yanayomkabiri, kulingana na NBC News.

Matatizo ya kisheria ya Combs yameongezeka baada ya shutuma zilizotolewa na aliyekuwa mpenzi wake Cassandra Ventura ‘Cassie’ mwezi Novemba lakini mapema mwaka huu, aliomba msamaha baada ya kufichuliwa kwa kanda iliyoonyesha akimshambulia mwanamke huyo katika ukumbi wa hoteli mnamo 2016.

Malalamiko yaliyowasilishwa na nyota wa zamani wa picha za utupu Adria English zinaeeza kwamba Diddy alimlazimisha mwanamke huyo kuingia katika biashara ya ngono.

Kesi hiyo mpya ipo katika jiji la New York inadai kuwa P-Diddy alimlazimisha English kujihusisha na biashara ya ngono kwa ajili yake huku rapa huyo akidaiwa kumtishia kuharibu kazi yake ikiwa hatafanya agizo lake.

Jumla ya mashtaka 33 yanatolewa dhidi ya Diddy na washirika wake katika jalada la English la kurasa 114, ambalo linatoa maelezo ya matukio kati ya 2004 na 2009.

“Haijalishi ni kesi ngapi zitawasilishwa lakini haitabadilisha ukweli kwamba Diddy hajawahi kudhalilisha kingono au kusafirisha mtu yeyote ngono,” wakili wake aliambia vyombo vya habari vya Marekani.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa “Bw Combs ana imani atashinda dhidi ya madai haya na mengine yasiyo na msingi mahakamani”.
Nyumba zake huko Los Angeles na Miami, Florida, zilivamiwa mapema mwaka huu kama sehemu ya uchunguzi wa serikali juu ya biashara ya binadamu.

Timu ya Combs imearifiwa kwamba yuko chini ya uchunguzi wa jinai unaoendelea wa shirikisho, kulingana na NBC News, ikinukuu vyanzo viwili vinavyofahamu masuala yake ya kisheria.

Related Articles

Back to top button