Mchanja atamani mkanda wa WBO ufike Ikulu

DAR ES SALAAM: BONDIA wa Ngumi za Kulipwa nchini na bingwa wa mkanda wa WBO Global, Yohana Mchanja amesema kuwa anatamani mkanda huo ufike Ikulu kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mchanja amefanikiwa kuubakiza mkanda huo nchini ikiwa ni mara ya kwanza kuwania ubingwa huo baada ya kushinda kwa pointi dhidi ya Miel Farjado wa Ufilipino pambano la raundi 12 uzito wa kati (kilo 56) pambano lilofanyika Desemba 26, jijini Dar es Salaam.
Mchanja amesema haikuwa kazi rahisi kushinda mkanda huo kutokana na mpinzani wake kuwa bora na kutokata tamaa.
“Mpinzani wangu alikuwa balaa , nilijaribu kutafuta kushinda KO imeshindikana na mbaya zaidi aliponidondosha katika raundi za mwanzo, sikukata tamaa na kujipa moyo kuwa nahitaji kupigana kwa ajili ya Taifa langu.
Nilifanikiwa kwa kumsoma mpinzani wangu na kutumia madhaifu yake kurudisha pointi zangu na nilifanikiwa kuuleta kwa mara ya kwanza mkanda wa ubingwa wa WBO Global, natamani sana mkanda huu ningeupeleka kwa Rais Samia ikiwa ni kumuonesha vijana wake tumekifanikisha alichotutuma,” amesema.
Mbali na mkanda huo wa WBO Global, mikanda mingine minne imefanikiwa kubakia kwenye ardhi ya Tanzania baada ya Ibrahim Mafia kushinda mkanda wa WBC baada ya kumchakaza kwa pointi, Lusizo Manzana wa Afrika Kusini.
Salmin Kassim alishinda mkanda wa WBF dhidi ya Adrian Lerasan ( Ufilipino), Kalolo Amiry a dhidi ya Sihle Jelwana ( India) kushinda mkanda wa PST na Said Chino alishinda mkanda wa IBA baada ya kumpiga, Malcom Klassen kutoka Afrika Kusini.