Michezo Mingine

Mbio za Ngalawa kutengewa fungu Kimataifa

ZANZIBAR: WIZARA ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar ipo katika hatua za mwisho kurasimisha mbio za Ngalawa/Jahazi kuingia katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ya Zanzibar, Aboud Suleiman Jumbe amesema mashindano ya Ngalawa ni sehemu ya Urithi wa Mambo ya Kale hivyo wizara hiyo itayafanya mashindano hayo yaendane sambamba na mashindano ya mbio za Kimataifa za boti za kisasa.

“Tupo katika mchakato wa kurasimisha mbio za ngalawa au jahazi kuwa katika ufadhili wa moja kwa moja kutoka wizarani na utawekewa mikakati ya kufanyika kuanzia ngazi ya kikanda, mikoa na kimataifa, lakini pia tunafanya mikakati ya mbio hizi Kwenda sambamba na mashindano ya mbio za boti za kisasa katika kikanda, kimkoa na kimataifa ili kuendana sambamba na mbio za boti za kisasa kitaifa na kimataifa.” alisema Jumbe

Jumbe amesema sekta ya Urithi wa Mambo ya Kale ni sekta mtambuka hivyo mashindano ya Ngalawa yanafuatiliwa na mataifa mengi na yamekuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Ngalawa 11 zilishindanishwa kila moja ikiwa na idadi ya watu saba hadi nane  ambapo Azam Marine iliibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia kitita cha Sh. Milioni 1, Cape Town Fish Market ikashika nafasi ya pili na kujishindia kitita cha Sh. 800,000 huku Robinson akishika nafasi ya tatu na akaondoka na Sh. 600,000. Washiriki wengine wa shindano hilo walipata kifuta jasho cha Sh. 100,000.

 

Mratibu wa mbio hizo Sabrina Faraja alisema mbio hizo ni utamaduni wa Mzanzibar kwa sababu zamani watu walikuwa wakitumia usafiri huo kabla ya kuibuka kwa teknolojia kubwa iliyoleta meli na boti.

“Usafiri wa Ngalawa kwetu ni sehemu ya utamaduni. Tunakumbuka usafiri uliokuwa ukitumika zamani ingawa sasa bado unatumika lakini kwa sasa kwa sehemu kubwa imebaki kuwa kama historia ya utamaduni wetu na ndiyo maana mashindano haya huwa yanafuatiliwa mno ndani na nje ya nchi” alisema Sabrina.

Related Articles

Back to top button