Martinez ajutia hasira zake dhidi ya uongozi wa Man United

MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa Manchester United, Lisandro Martinez, amesema hasira na kukatishwa tamaa kufuatia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Atletico Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ndizo zilizomfanya kuukosoa uongozi wa klabu hiyo kwa kile alichodai kuwa ni uwekezaji mdogo katika usajili wa wachezaji.
United ilipoteza mchezo huo nchini Hispania siku ya Jumanne, huku ikiendelea kukabiliwa na mwanzo mgumu wa msimu katika Ligi Kuu ya England, ikiwa ni mwanzo wake mbaya zaidi kwa takribani miaka 40.
Martinez alikuwa amemkosoa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo, Jason Wilcox, akisema alitarajia klabu kufanya uwekezaji mkubwa zaidi katika dirisha la usajili baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu msimu uliopita na kurejea katika michuano ya Ulaya.
Katika dirisha hilo la usajili, Manchester United ilisajili viungo watatu, Carlos Baleba, Youri Tielemans na Andrey Santos, kwa gharama inayokadiriwa kufikia pauni milioni 150, sawa na takribani dola milioni 198 za Marekani. Hata hivyo, matumizi hayo yalikuwa chini ya yale ya baadhi ya wapinzani wake katika Ligi Kuu.
Akifafanua kauli yake kupitia mitandao ya kijamii, Martinez alisema alizungumza akiwa na hasira na kukatishwa tamaa baada ya timu hiyo kushindwa kupata matokeo iliyokuwa ikiyatarajia.
“Baada ya mchezo, nilizungumza kutokana na hasira na kukatishwa tamaa kwa kutopata matokeo ambayo sote tuliyataka,” alisema Martinez.
Kauli za beki huyo wa kimataifa wa Argentina ziliungwa mkono na baadhi ya mashabiki, lakini pia amekosolewa kutokana na mchango wake katika matokeo mabaya ya United mwanzoni mwa msimu huu.
Martinez alijifunga bao katika sare ya 1-1 dhidi ya Fulham mwezi uliopita, kabla ya kushindwa kuzuia nguvu ya Dominic Solanke katika mchezo ambao Tottenham, ikiwa na wachezaji 10, ilipata sare dhidi ya United katika uwanja wa Old Trafford mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akijibu ukosoaji huo, Martinez alisisitiza kuwa matamanio yake ni kuona klabu hiyo ikiendelea kukua na kuwa na uwezo wa kushindana katika kiwango cha juu.
Alisema viwango vya juu vinapaswa kuzingatiwa na kila mtu ndani ya klabu, akiwemo yeye mwenyewe, na kuongeza kuwa ana imani na wachezaji wenzake, kocha na wafanyakazi wanaojitahidi kuirejesha United katika mafanikio.
Martinez alisisitiza kuwa njia ya kuisogeza klabu mbele ni kuendelea kufanya kazi kwa pamoja, kwa kujituma na kuwa na malengo makubwa.
Wakati huo huo, presha inaendelea kuongezeka kwa kocha wa Manchester United, Michael Carrick, miezi michache tu baada ya kupewa nafasi hiyo kwa mkataba wa kudumu.
Carrick na kikosi chake wanatarajiwa kusafiri kwenda kukutana na wapinzani wao wa kihistoria, Leeds United, siku ya Jumapili katika Ligi Kuu ya England.
Baada ya mchezo huo, United itasafiri tena kwa ajili ya kukabiliana na Como ya Italia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya siku ya Jumatano.
Matokeo ya michezo hiyo yanatarajiwa kuwa muhimu kwa United katika juhudi za kurekebisha mwenendo wake wa msimu huu na kupunguza presha inayozidi kuongezeka kwa benchi la ufundi.




