Kenya yapokea milioni 335 kutoka CAF, FIFA mwaka huu

NAIROBI, KENYA: SHIRIKISHO la Soka Kenya (FKF) linatarajiwa kunufaika na ufadhili kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), huku fedha hizo zikilenga kuimarisha maendeleo ya soka nchini humo.
CAF imeongeza ruzuku ya mwaka kwa kila chama mwanachama kutoka dola za Marekani 525,000 hadi dola 700,000, ongezeko la asilimia 33.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha maendeleo ya soka, kuwekeza katika soka la vijana na wanawake, pamoja na kuboresha usimamizi wa vyama vya soka.
Kwa upande wa FIFA, FKF inastahili kupokea jumla ya dola milioni 9.2 katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2022 hadi 2026 kupitia mpango wa maendeleo wa FIFA Forward 3.0.
Fedha hizo zimegawanywa katika maeneo mbalimbali, yakiwemo gharama za uendeshaji, miradi ya maendeleo na mahitaji ya timu za taifa. Kati ya fedha hizo, dola milioni tano zimetengwa kwa gharama za uendeshaji, dola milioni tatu kwa miradi maalumu ya maendeleo, huku dola milioni 1.2 zikielekezwa katika usafiri, malazi ya timu za taifa na vifaa vya soka.
Katika hatua nyingine, FKF imepanga kujenga kituo kipya cha kiufundi katika Kaunti ya Machakos, mradi unaokadiriwa kugharimu takribani shilingi za Kenya milioni 600.
Kituo hicho kinatarajiwa kusaidia kuboresha miundombinu ya soka, maandalizi ya wachezaji na maendeleo ya vipaji nchini humo.
Aidha, maendeleo ya soka la wanawake ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kunufaika na ufadhili wa FIFA, kupitia programu za kuimarisha ligi, kuwajengea uwezo makocha na wasimamizi, pamoja na kuboresha maandalizi ya timu za taifa za wanawake.
Ufadhili kutoka CAF na FIFA ni sehemu muhimu ya juhudi za kuimarisha soka nchini Kenya. Hata hivyo, mafanikio ya mipango hiyo yatategemea usimamizi wa fedha na utekelezaji wa miradi iliyopangwa.




