Azam mguu sawa CAFCL
DAR ES SALAAM, MTENDAJI Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, ameeleza mikakati ya msimu ujao kutaka kufikia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na SpotiLeo Popat amesema wameanza mapema maandalizi ya michuano hiyo kwa kufanya usajili wa wachezaji wapya mapema na ndani ya siku mbili hizi watatambulisha nyota wapya wawili kwa ajili ya kuboresha timu yao kwa msimu ujao wa michuano hiyo.
Safari ya Azam FC kuisaka nafasi ya kushiriki ya Mabingwa Afrika msimu huu imefanikiwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Gold, kumaliza Ligi Kuu Bara ikiwa nafasi ya poli katika msimamo.
Popat amesema licha ya kuwepo kwa kibarua mbele yao mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho la CRDB Bank dhidi ya Yanga, lakini wameangalia jinsi ya kuanza maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mapema kwa kuongeza baadhi ya nyota wapya.
Ameeleza kuwa mipango ya michuano ya Ligi ya Mabigwa Afrika kwa msimu ujao, yameanza mapema baada ya kukamilisha usajili wa nyota wapya watatu akiwemo kiungo kutoka klabu ya Leonnes ya Colombia, Ever Meza na mshambuliaji Jhonier Blanco
“Tunatambua hii michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika sio rahisi tutaenda kukutana na timu bora kwa kufahamu tumeanza maandalizi ikiwemo kusajili aina ya wachezaji wanaopendekezwa na kocha Youssouph Dabo.
Tunatambua ugumu wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tunatakiwa kujipanga vizuri, kufanya usajili wachezaji bora watakakaokuja kuleta ushindani mkubwa na kufikia malengo yetu ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo hatukuwa kufika hapo awali,”amesema Popat.
Amesema msimu huu wanajiandaa vizuri kwa kufanya usajili mzuri kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi kwa kuimarisha kikosi cha timu yoa kufikia malengo waliyojiwekeza ya kucheza hatua ya makundi.
Azam FC iliyoanzishwa mwaka 2004 na kuanza Ligi Kuu Bara 2008 iliwahi kufanikiwa kushiriki michuano ya Ligi ua Mabingwa Afrika mara moja tu mwaka 2014 baada ya msimu wa 2013/3014 kuwa Mabingwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tangu 2014, Azam FC ilikuwa ikisaka nafasi ya kushiriki ligi ya Mabingwa Afrika lakini ikiwa inajikuta ikiangukia kombe la Shirikisho la Afrika.