Mastaa

Shah Rukh Khan aonya vurugu atangaza amani

INDIA: MWIGIZAJI maarufu wa Bollywood, Shah Rukh Khan, ametoa wito wa mataifa na jamii mbalimbali kutanguliza mazungumzo badala ya vurugu, akisisitiza kuwa amani huanza ndani ya mioyo ya watu.

Akizungumza katika hafla ya Global Peace Honours iliyofanyika jijini Mumbai Jumamosi, nyota huyo alihimiza watu kuchagua kuaminiana badala ya hofu na kuimarisha mshikamano ili kuondoa chuki na kujenga upendo.

Shah Rukh Khan alisema amani si jambo la kusubiri litokee lenyewe, bali ni uamuzi, wajibu na ahadi ambayo kila mmoja anapaswa kuitimiza kila siku.

Akisimulia mazungumzo aliyowahi kuwa nayo na mwanawe mdogo kuhusu namna chuki inavyoweza kubadilishwa kuwa upendo, mwigizaji huyo alisema suluhisho ni watu kuchagua mazungumzo badala ya kutumia nguvu na kujifunza kuishi kwa maelewano.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa watu kuelewa mitazamo na simulizi za wengine hata pale wanapokuwa hawakubaliani kuhusu kila jambo.

Katika hafla hiyo, Shah Rukh Khan pia aliwakumbuka waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi, yakiwemo mashambulizi ya Mumbai ya Novemba 26, 2008 na shambulizi la Pahalgam, huku akitoa heshima kwa maafisa wa usalama waliopoteza maisha wakilinda nchi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Maharashtra, Devendra Fadnavis, na kuandaliwa na Divyaj Foundation inayoongozwa na mkewe, Amruta Fadnavis.

Akihitimisha ujumbe wake, Shah Rukh Khan alitoa wito kwa wananchi kuungana na kutambua kuwa kila mtu ana jukumu la kulinda amani, mshikamano na ustawi wa jamii.

Related Articles

Back to top button