Kaze aanza kazi Kagera Sugar Sugar

KAGERA: KOCHA Mkuu mpya wa Kagera Sugar, Cedric Kaze, amesema ushirikiano kati ya uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki ndiyo msingi wa kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri katika msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kaze amesema hayo jana baada ya kutambulishwa rasmi kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, akichukua nafasi ya Juma Kaseja aliyeachwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo katika mechi sita zilizopita.
“Ninaamini kama tukishirikiana sote, kuanzia uongozi wa timu, benchi la ufundi hadi wachezaji na tukipata sapoti ya mashabiki wetu tunaweza kufanya vitu vizuri na kuwafurahisha,” amesema Kaze.
Kaze, raia wa Burundi, anarudi Tanzania akiwa na uzoefu wa soka la ndani na nje ya nchi, baada ya kuwahi kufanya kazi katika klabu ya Yanga kama Kocha Msaidizi chini ya Nasreddine Nabi, baadaye kama Kocha Mkuu kabla ya kuendelea na majukumu ya ukocha nchini Afrika Kusini.
Kocha huyo pia amewahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Kaizer Chiefs na baadaye kuwa kocha mkuu wa Sekhukhune United, hatua iliyompa uzoefu wa kufanya kazi katika mazingira tofauti ya soka.
Kaze anakabidhiwa Kagera Sugar ikiwa katika kipindi ambacho timu hiyo inahitaji kuboresha matokeo yake, huku akipewa jukumu la kuijenga upya na kuipeleka katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Kwa sasa Kagera Sugar inashika nafasi ya pili kutoka mwisho katika michezo sita, ikiwa haijashinda mchezo wowote zaidi ya kupata sare mbili na kupoteza michezo minne ikiwa na pointi mbili.
Kocha huyo mwenye leseni ya ukocha ya CAF daraja A pamoja na leseni ya daraja A ya Shirikisho la Soka la Ujerumani, anatarajiwa kuanza kazi mara moja kuelekea michezo ijayo ya timu hiyo.




