Burudani

Rais Samia atenga sh. bilioni 450 kwa ajili ya arena na kijiji cha filamu

Rais Samia atenga sh. bilioni 450 kwa ajili ya arena na kijiji cha filamu

DAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amejibu wito wa staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, kwa kukubali kufadhili ujenzi wa uwanja wa kisasa wa matamasha pamoja na Kijiji cha Filamu nchini Tanzania.

Katika Tamasha la Tuzo za Trace Music lililofanyika hivi karibuni visiwani Zanzibar, changamoto za miundombinu zilijitokeza wazi, hasa baada ya jukwaa la tamasha hilo kushindwa kuwa imara, jambo lililozua hofu kwa wasanii waliokuwa wakitumbuiza. Kufuatia tukio hilo, Diamond aliitaja hali hiyo kuwa aibu kwa nchi mwenyeji.

Tamasha hilo liliwaleta pamoja wageni mashuhuri, wakiwemo wasimamizi wakuu wa muziki wa kimataifa, marais wa lebo za rekodi mbalimbali, na watayarishaji wa kazi za muziki kutoka mataifa yaliyoendelea katika sekta hiyo.

“Trace walihangaika kuandaa jukwaa Zanzibar, lakini liliendelea kusambaratika. Ilikuwa ya kufedhehesha, hasa kwa kuzingatia idadi ya wageni wa kimataifa waliohudhuria,” alisema Diamond baada ya tamasha hilo.

Pia, aliitaka serikali kuwekeza katika uwanja wa kisasa ili kuepuka matatizo kama hayo siku za usoni. “Tunahitaji miundombinu bora ili kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji. Kilichotokea kwa Trace kinaweza kuwakatisha tamaa wasirudi tena,” alisisitiza.

Msemaji wa Serikali ya Tanzania, George Msigwa, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni, amethibitisha kupatikana kwa fedha za mradi huo.

“Rais hivi karibuni alipata mkopo nafuu wa dola bilioni 2.5 kutoka Korea Kusini. Kati ya fedha hizo, sh bilioni 450 (dola milioni 172) zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wa matamasha na Kijiji cha Filamu. Diamond amelizungumzia suala hili mara kadhaa, akisisitiza kwamba wakati serikali inawekeza kwenye viwanja vya soka, mahitaji ya wanamuziki yamepuuzwa kwa muda mrefu,” alieleza Msigwa.

 

 

Related Articles

Back to top button