Ligi Daraja La Kwanza

Geita, TMA hazijachana nyavu zao

DAR ES SALAAM: Timu za Championship za Geita Gold na TMA ndizo timu pekee ambazo nyavu zao hazijaguswa kwenye Ligi hiyo katika michezo sita waliyocheza mpaka sasa.

Geita ambao ni vinara kwa pointi 14 katika michezo sita, wameshinda minne na sare mbili, wakiwa hawajapoteza mchezo huku TMA wakishinda mitatu na sare tatu nao pia hawajapoteza mchezo wakishika nafasi ya tatu kwa pointi 12 nyuma ya Mtibwa Sugar katika nafasi ya pili kwa pointi 13, ambaye amepoteza mchezo mmoja.

Kazi ipo katika mechi zijazo je, wataweza kuendelea kulinda nafasi zao? Wakiteleza kidogo walioko chini wanapishana nafasi zao kutokana na utofauti mdogo wa pointi wanazotofautiana.

Kinara Geita katika mchezo ujao Jumapili atakuwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kumenyana na Mbeya Kwanza katika mchezo ambao huenda ukawa mgumu kutokana na ubora wa kila moja.

Pia, nafasi ya pili Mtibwa Sugar itakuwa kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro Jumamosi kumkaribisha Songea United inayofundishwa na kipa wa zamani wa Simba na Yanga Ivo Mapunda huku TMA ikitarajiwa kucheza na Mbuni mkoani Arusha Jumapili.

Matokeo ya mechi hizi yanaweza kubadilisha msimamo au ukabaki kama ulivyo.

Related Articles

Back to top button