Fei toto aiwaza Azam hatua ya makundi Ligi ya mabingwa
DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, amesema wana deni kubwa la kucheza hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo wanashiriki sasa.
Amesema wanatambua umuhimu wa michuano hiyo na wanahitaji kuweka rekodi yao ya kucheza makundi ya Afrika kwa kuendelea kutafuta ushindi mchezo wa marudiano dhidi ya APR ya Rwanda.
Kikosi cha matajiri wa Chamazi, Azam FC, kimewasili nchini Rwanda kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wa APR, unaochezwa Jumamosi Agosti, 24, uwanja wa Amahoro, nchini.
Fei Toto ameliambia spotileo, malengo makubwa ni kuona timu inapiga hatua kubwa kwa kucheza hatua ya makundi ambayo hawajawahi kufikia na kuishia katika mechi za awali.
“Tumekuja kupambana kutafuta ushindi dhidi ya APR, hautakuwa mchezo rahisi tutapambana kuvuka hatua hii ya mkondo wa kwanza na kusonga mbele, tunataka kucheza makundi safari hii,” amesema Fei Toto.
Ameeleza kuwa kulingana na usajili uliofanywa, wana kila sababu ya kufanya vizuri katikia michuano ya Afrika, pamoja na kuhitaji kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita.
Azam Fc wanahitaji sare ya aina yoyote ili kusonga hatua inayofuata ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika huko APR wanahitaji kushinda goli kuanzia 2 – 0 ili wafuzu.