Ligi Kuu

Farid Mussa: Majeraha yamenipa wakati mgumu

KIUNGO wa Yanga, Farid Mussa amesema kitendo cha kupata majeraha ya kuchanika nyuma ya goti kilimpa wakati mgumu na haikuwa rahisi kwake kuamini kama angerejea haraka kujiunga na wenzake.

Nyota huyo hakuonekana sana msimu huu kutokana na kuchanika kwa misuli nyuma ya goti hali iliyosababisha kufanyiwa upasuaji tangu mwezi uliopita.

Akizungumza Dar es Salaam nyota huyo amesema daktari alimkatisha tamaa kwa kumwambia kuwa kupona kwake kungechukua miezi mitatu hadi Desemba. Mchezaji huyo anaendelea vizuri na tayari ameanza mazoezi mepesi kujiweka imara.

“Haikuwa rahisi kwangu hasa pale ambapo niliambiwa ingechukua muda mrefu kupona kwasababu kama mchezaji napenda kufanya mazoezi na wenzangu na kucheza, nashukuru Mungu nimerejea mapema,”amesema.

Amesema alipopata ajali mwanzoni alikataa kufanyiwa upasuaji kwa kuhofia pengine ingemchelewesha kupona ila baadaye alikubali baada ya kushauriwa na daktari.

Daktari wa timu hiyo Moses Itutu amesema imechukua muda wa wiki mbili kidonda cha Farid kufunga kutokana na kufuata masharti aliyompa na ameanza mazoezi mepesi, hana maumivu yoyote kwani anaweza kukimbia.
Amesema hajamruhusu kucheza akihofia anaweza kutonesha kidonda anasubiri mpaka apone vizuri atarejea kama zamani.

Related Articles

Back to top button