Ligi Kuu

Fadlu kuwakosa nyota wawili

ARUSHA: KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amethibitisha kuwa kikosi chake kitawakosa nyota wawili, kipa Moussa Camara na beki Che Malone Fondoh, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, utakaochezwa Jumamosi, Machi Mosi, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Kikosi cha Simba kimeondoka leo asubuhi kuelekea Arusha kwa ajili ya mchezo huo, huku Camara na Fondoh wakibaki Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo vya afya baada ya kuumia kwenye mechi iliyopita dhidi ya Azam FC.

“Hawatakuwa sehemu ya mchezo wa kesho. Ni wachezaji wazuri na muhimu kwa timu, lakini hatuna presha. Kutakuwa na mabadiliko madogo kwenye kikosi baada ya kukosekana kwao,” amesema Fadlu.

Kocha huyo amesema bado hajapata taarifa rasmi juu ya muda ambao nyota hao watakuwa nje ya uwanja, lakini anaamini baada ya vipimo atajua ukubwa wa majeraha yao.

Akizungumzia maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Coastal Union, Fadlu amesema anatarajia mechi kuwa ngumu, hasa kutokana na matokeo ya mzunguko wa kwanza ambapo timu hizo zilitoka sare kwenye Uwanja wa KMC Complex.

“Tumejiandaa kama ilivyo kwenye michezo mingine. Tumefanyia kazi mapungufu yetu kupitia makosa tuliyofanya kwenye mechi za nyuma, hasa dhidi ya Azam FC,” amesema Fadlu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button