Kwingineko

CR7 kusalia Al Nassr hadi atakapofikisha miaka 42

RIYADH, Saudi Arabia: NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, ameongeza mkataba wa kusalia Al Nassr hadi mwaka 2027, hatua inayoendelea kuonesha dhamira yake ya kuendelea kucheza soka la ushindani licha ya umri wake kufikia miaka 40.

Taarifa hiyo imethibitishwa kupitia ukurasa rasmi wa Ronaldo kwenye Instagram, ambapo alichapisha picha akiwa na jezi ya Al Nassr sanjari na kigogo wa Klabu hiyo na kuandika kwa kifupi:

“Sura mpya inaanza. Shauku ileile, ndoto ileile. Tuiandike historia Pamoja.”

Kwa mkataba huo mpya, Ronaldo anatarajiwa kubaki katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia hadi atakapofikisha takribani miaka 42, ikiwa ni muendelezo wa safari yake ya kipekee ya soka iliyopita katika vilabu vya Sporting Lisbon, Manchester United, Real Madrid na Juventus.

Safari ya Ronaldo kuelekea Saudi Arabia mwaka 2022 uligusa mioyo ya watu wengi duniani huku wakijiuliza kimemkuta nini? kuendelea kwake na Al Nassr hadi 2027 ni ujumbe tosha kuwa soka la Kiarabu linaendelea kukua kwa kasi.

Mashabiki wa Al Nassr wamefurika kwenye ukurasa wa mchezaji huyo mwenye wafuasi wengi duniani zaidi ya milioni 635 huku wengi wakifurahia taarifa hiyo, wakiamini kuwa Ronaldo ataendelea kuwa chachu ya mafanikio ndani na nje ya uwanja.

Related Articles

Back to top button