CMB Prezzo afafanua alivyokuwa akiwavutia warembo

NAIROBI: RAPA kutoka Kenya CMB Prezzo ameweka wazi namna alivyokuwa akifanikiwa kuwa na uhusiano na wanawake warembo na wenye majina makubwa ndani na nje ya Kenya.
Prezzo ameeleza hayo katika kipindi cha Oga Obinna baada ya kuibuka mjadala ambapo Obinna aliuliza namna alivyoweza kuvutia wanawake wa aina hiyo.
“Unajua, mimi ni mtu mpole. Unapozungumza kwa upole na unyoofu kwa wanawake, wanaweza kufikiria kuwa unatania wakati namaanisha kila kitu ninachosema,” Prezzo alieleza. “Sijisikii wala sijikwezi nadhani ndiyo sababu ninashinda, sijawahi kushindwa.”
Prezzo aliendelea kueleza kuwa mwanamke ni muhimu hivyo unapotaka kuwa naye lazima uanze kuchukua hatua.
“Msome kwanza. Tengeneza fomula, fanya hesabu utapata jibu sahihi, utajua nini cha kufanya na nini usifanye,” alishauri Prezzo.
Prezzo alisema wanawake wengine walikuwa wakipendezwa na maadili ya kazi yake: “Sheila alipendezwa na maadili ya kazi yangu. “Mimi si wa kuangalia maigizo ila kuna wakati tungetazama filamu, tukala popcorn, na kisha mengine yakaendelea,” Prezzo alifafanua.
Alipoulizwa kwa nini uhusiano na mwanamke huyo uliisha, alitoa jibu la kifalsafa:
“Katika maisha, mambo hutokea. Ninaamini Mungu huwaweka watu katika maisha yetu kwa sababu. Sheila alikuwepo kunisaidia wakati huo, na jukumu lake lilipotimizwa, maisha yalisonga mbele, hivyo ndivyo ilivyo.”