Chuwa amtishia Ndame kipigo cha KO

DAR ES SALAAM: BONDIA John Chuwa ameongeza makali ya vita ya maneno kuelekea pambano lake dhidi ya Nassoro Ndame, akiahidi kumtwanga kwa KO katika pambano la Boxing Day litakalofanyika Desemba 26, 2026, jijini Dar es Salaam.
Chuwa amesema amemsikia mpinzani wake akitoa kauli mbalimbali, lakini amesisitiza kuwa hawezi kutishwa wala kuogopeshwa na maneno hayo, akidai kuwa maandalizi yake yamekamilika kiakili na kimwili.
Akizungumza leo wakati akiendelea na maandalizi yake, Chuwa amesema anaamini Ndame hana uwezo wa kumshinda, huku akimtaka aendelee kuzungumza kwa sababu majibu yake atayatoa ndani ya ulingo.
“Nimemsikia Nassoro Ndame, lakini hawezi kunishinda. Nimeshampiga mtu kwa KO, hivyo achonge tu maneno. Nimejiandaa kikamilifu, tarehe 26 hawezi kumaliza pambano. Sijawahi kumuogopa wala kumhofia, nimejiandaa kiakili na kimwili,” amesema Chuwa.
Ameongeza kuwa anachomwambia Ndame ni kujiandaa kukabiliana na kipigo kikali, akidai kuwa pambano hilo litakuwa na wakati mgumu kwa mpinzani wake.




