Bondia wa Tanzania kupimwa ubavu na Mnigeria

LAGOS: BONDIA Mtanzania Suleiman Sheha anatarajiwa kupigana na bondia wa Nigeria, Basit Adebayo maarufu ‘Jokerboy’ kuwania taji la Kimataifa la WBO Youth uzito wa Lightweight.
Pambano hilo litafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Balmoral nchini Nigeria mnamo Aprili 18.
Kwa mujibu wa Dk. Ezekiel Adamu muandaaji wa pambano hilo kwa kushirikiana na Game Rush Pamoja na Balmoral Promotions, pambano hilo ndilo litakuwa pambano kuu likiwa na utangulizi wa mapambano mengine na mabondia kutoka taifa la Ghana, Misri, Italia na Uingereza.
Waandaji wa tukio hilo walilolipa jina la ‘Chaos in the Ring’, wamesema wamelenga kukusanya Naila milioni 50 ili kusaidia programu za maendeleo ya jamii zinazozingatia elimu, afya na uwezeshaji wa kiuchumi.
Pambano hilo litaburudishwa na utangulizi wa wasanii wa muziki na vichekesho nchini humo kwa kupigana ulingoni ili kumpata mbabe wa majigambo na ulingoni.