Aussems: Hao Ken Gold waje tu!
DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Patrick Aussems amesema amewatazama, Ken Gold FC na kudai kuwa timu yake kiufundi ipo vizuri na wapo tayari kwa msimu wa 2023/24 wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Ligi hiyo itarajiwa kuanza kutimua vumbi Ijumaa, Agosti 16, 2024, Singida Black Stars wataanzia ugenini dhidi ya Ken Gold, wikiendi, uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Akizungumza na Spotileo, Aussems amesema wamefanya maandalizi ya wiki tano hadi sita, umefika muda wa kufanyia kazi kile walichokifanya katika uwanja wa mazoezi.
Amesema kila mchezaji anatamani kuanza msimu mpya wa ligi na wanatambua kuanza mchezo huo ugenini kwa kuhitaji kupambana kutafuta pointi tatu muhimu dhidi ya Ken Gold.
“Vijana wangu wapo vizuri tunaenda kucheza na Ken Gold kiufundi tupo vizuri zaidi ya wapinzani wetu, kikubwa wachezaji wanatakiwa kutuliza akili na kupambana kutafuta matokeo chanya ugenini,” amesema Aussems.
Amesisitiza kuwa wanatakiwa kuwa makini na kuingia katika mchezo huo kwa nidhamu kwa sababu mpira unadunda na wanaweza kuadhibiwa kwa kufanya makosa.