Asake aweka rekodi 02 Arena, Uingereza kama Davido, WizKid

LONDON: MWANAMUZIKI wa Nigeria, Asake ameweka rekodi ya kuuza tiketi zote za Ukumbi wa O2Arena uliopo London nchini Uingereza.
Mwanamuziki huyo wa Afrobeat aliyeshinda tuzo ya MOBO, amefanikisha rekodi yake hiyo kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2023 alipotoa albamu yake ya pili ‘Work of Art’.
Asake, amepata mafanikio makubwa kwa kuuza tiketi katika Ukumbi wa O2 Arena wenye uwezo wa kuchukua watu 20,000, kwa mara ya pili ndani ya miaka miwili.
Kujaza Ukumbi mkubwa wa O2 Arena, uliopo London, Uingereza ni hatua muhimu mno kwa msanii yeyote duniani. Hatua ya kuuzwa kwa tiketi zote ni uthibitisho wa umaarufu wa msanii na hitaji kubwa la muziki wake kwa mashabiki wake duniani kote.
Mafanikio ya Asake ya kuuza tiketi zote katika ukumbi huo mara mbili ndani ya miaka miwili yanamweka katika uwiano sawa na nyota wa kimataifa kama vile Beyonce, Spicegirls, Rihanna na Rolling Stones, ambao pia wamewahi kuuza tiketi zote za ukumbi huo katika maonyesho yao.
Lakini pia katika rekodi yake mwanamuziki huyo pia anaungana na wanamuziki wengine wa Nigeria Davido na Wizkid, ambao nao waliwahi kuuza tiketi zote na kuujaza ukumbi huo wa O2 Arena kwa zaidi ya mara moja.
Asake alitumbuiza kwa mafanikio katika ukumbi huo wa 02 Arena kama sehemu ya ziara yake ya ‘Lungu Boy World Tour’ ambapo katika shoo yake aliingia kiaina huku umati wa watu waliojaa katika ukumbi huo walilipuka kwa shangwe wakiimba kwa pamoja nyimbo za msanii huyo ukiwemo wimbo wa ‘Olorun’, ‘Omo Ope’ na ‘Amapiano’.