“Andaeni mkakati wa kuendeleza vituo vya michezo” – Majaliwa
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu wa Jamhuri Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Utamaduni Sanaa na michezo kuandaa mpango mkakati wa kuwepo kwa vituo vya kukuza na kendeleza michezo vinavyojitegemea ili kukuza vipaji vya wachezaji wazawa.
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu ni baada ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia kufafanua juu ya idadi ya wachezaji wakigeni kumewafanya wazawa kuondoa uoga wa kucheza na nyota wenye majina makubwa na kusaidia timu kufanya vizuri katika michuano ya Afrika kwa kucheza robo fainali kwa Simba na Yanga kwa msimu mmoja.
“Kuwepo kwa vituo hivyo kusaidia kupatikana kwa timu bora za Taifa kwa sababu ya wachezaji hao kupata misingi bora tangu chini. Pia kuwepo kwa elimu ya juu ya makocha wetu,” amesema Waziri mkuu Majaliwa.
Waziri mkuu pia amesema kuwa idadi ya wachezaji 12 wa kigeni sio mbaya kwa sababu inawapa wazawa changamoto ya kutafuta nafasi ya kucheza ndani ya timu kulingana na ushindani utakaokuwepo.
“Maendeleo ya wenyewe kwa wenyewe hayawezi kuwa, tuna wachezaji wazuri lakini hawajitumi uwanjani hii inatokana na kutokuwa na misingi kuanzia chini lakini wakiwepo hawa wageni na tunapokuwa na vituo vya michezo inasaidia kupata wachezaji bora na timu za taifa imara,” amesema.
Waziri mkuu amesema kufungua milango ya wachezaji wa kigeni imewezesha Tanzania kuwa sehemu ya kimbilio la nyota hao kutamani kucheza, jambo ambalo linaongeza ubora wa ligi.
“Tuwe tunapokea wachezaji wakigeni lakini pia tunahakikisha na wachezaji wetu wanafanikiwa kwenda kucheza soka la ushindani nje ya nchini,” amesema Waziri Majaliwa.