Ligi Kuu

Ahmed Awapa Siri Azam FC Kuhusu Ahoua

DAR ES SALAAM: Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa mtaalamu wao wa kupiga penalti, Jean Ahoua, yupo makini na kazi yake. Ametoa onyo kwa mabeki wa Azam FC kuhakikisha hawafanyi makosa ndani ya boksi katika mchezo wao wa Mzizima Derby.

Simba watakuwa wenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Jumatatu, Februari 24, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Ahmed amesema kuwa wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa wamekamilika kwa asilimia 100 na wanaomba Mungu asitokee mchezaji yeyote kuumia kabla ya siku ya mechi.

“Niwakumbushe tu Azam FC, wachezaji wetu wameongezeka ubora mara dufu zaidi ya walivyocheza mchezo wa kwanza. Ukimuangalia Abdulrazack (Hamza), yupo vizuri zaidi, na Azam wasifanye makosa ndani ya boksi kwa sababu mtaalamu wetu wa penalti, Jean Ahoua, atawaumiza,” amesema Ahmed.

Ameeleza kuwa Simba inautazama mchezo huo kama moja ya mechi muhimu sana kwa msimu huu kwa sababu matokeo yake yanaweza kuonesha dira ya mafanikio yao. Ili kupata mafanikio wanayokusudia, lazima waifunge Azam FC.

“Lakini huu ni mchezo mgumu kwa sababu tunacheza na timu ambayo tunalingana nayo kwa ubora. Simba na Azam FC tunafanana kwa kila kitu – ubora wa wachezaji, uwekezaji na hata viwango vya timu. Ni timu mbili zinazolingana na zinakutana siku ya Jumatatu,” amesema Ahmed.

Amesema kuwa tofauti kubwa kati ya timu hizo ni umakini, ambapo Simba inaonekana kama timu kubwa zaidi, huku Azam FC ikiendelea kujijenga. Kwa sababu hiyo, Simba wameingia kambini mapema zaidi kuhakikisha wanajipanga kikamilifu kwa mchezo huo.

“Ili tujiweke kwenye mazingira mazuri ya kushinda ubingwa msimu huu, hatuna budi kuifunga Azam FC inayoshika nafasi ya tatu na kisha Machi 8 kumfunga timu inayoshika nafasi ya pili. Kwa upande wetu Simba, tumeanza mikakati kabambe kuhakikisha tunapata ushindi katika michezo hii,” amesema Ahmed.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button