Habari Mpya

Andambwile atia timu kwa Wananchi

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imekamilisha usajili wa kiungo mkabaji, Aziz Andambwile anaetarajia kukitumikia kikosi  hicho kwa mkataba wa mwaka mmoja hadi Julai 2025 kwenye timu hiyo yenye ushindani mkubwa ndani ya Ligi Kuu Bara.

Ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema usajili wa kiungo huyo ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Miguel Gamondi ambaye anahitaji kuimarisha kikosi cha Yanga.

Nyota huyo amejiunga na Yanga akitokea Singida Fountain Gate FC na anaenda kuongeza nguvu eneo ambalo linachezwa na Khalid Aucho na Jonas Mkude.

“Tumefanikiwa kumsajili kiungo huyo baada ya kuridhishwa na uwezo wake ataongeza nguvu eneo hilo na anatarajia kuungana na wachezaji wenzake kambini mapema kujiandaa na msimu mpya,” amesema Kamwe.

Amesema wanaimani na uwezo wa kiungo huyo baada ya kufanya vizuri timu aliyotoka, ana uwezo mkubwa wa kuzuia timu ikishambuliwa na yupo kwenye mipango ya Kocha Gamondi katika michuano iliyopo mbele yao.

Amesema wanatarajia kuondoka nchini kuelekea Afrika Kusini na kucheza mechi za kirafiki ikiwemo dhidi ya Kaizer Chief ya nchini humo, mchezo huo ukiwa ni sehemu yao ya kujipima.

“Wachezaji wa kimataifa wameanza kuwasili nchini na kupima afya na kuwa tayari kwa ajili ya msimu ujao, tutaweka kambi ya muda mfupi jijini Dar es Salaam na baadae tutaenda Afrika kusini kwa ajili ya mchezo wetu huo,” amesema Ofisa habari huyo

Related Articles

Back to top button