CAF: AFCON 2027 kuitangaza Afrika Mashariki duniani

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limesema Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Afrika Mashariki kimataifa kupitia soka, utalii, utamaduni na ukarimu wa wananchi wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Katibu Mkuu wa CAF, Samson Adamu, amesema ushirikiano wa AFCON Pamoja 2027 una lengo la kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa na manufaa makubwa zaidi ya mchezo wa soka kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi hizo tatu.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ushirikiano kati ya CAF na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), unaolenga kuitangaza Tanzania kupitia mashindano ya AFCON 2027, Adamu amesema nchi hizo zina vivutio vingi vinavyoweza kuwavutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
“Tanzania ina utajiri mkubwa wa vivutio vya utalii, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro na fukwe za Zanzibar, mashindano hayo yatatoa fursa ya kuonesha uzuri huo kwa hadhira ya kimataifa,”amesema.
Adamu amesema CAF inataka mashabiki waje kwa ajili ya soka lakini wabaki kutokana na uzoefu watakaoupata katika nchi hizo, ikiwemo kukutana na watu, kujifunza tamaduni na kufurahia ukarimu wa wenyeji.
Ameongeza kuwa mafanikio ya AFCON 2027 hayatapimwa kwa ubora wa mashindano pekee, bali pia kwa mahusiano yatakayojengwa, kumbukumbu zitakazoundwa na wageni watakaovutiwa kurejea Afrika Mashariki hata baada ya mashindano kumalizika.
Amesema ushirikiano huo unaendana na maono ya Rais wa CAF, Patrice Motsepe, ya kuhakikisha mpira wa miguu unachangia kwa vitendo maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
Adamu amesisitiza kuwa Tanzania, Kenya na Uganda hazijiandai tu kuandaa mashindano ya soka, bali zinajiandaa kuipokea dunia na kuonesha uwezo, utamaduni na ukarimu wa Afrika Mashariki.




