AFCON

Makonda: AFCON 2027 kuingiza Sh trilioni tano

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yanatarajiwa kuchochea mzunguko wa fedha unaokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni mbili, sawa na zaidi ya Sh trilioni tano, katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Makonda amesema mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa siku 29, yakihusisha timu 24 na mechi 52, si tukio la kimichezo pekee, bali ni fursa ya kukuza uchumi, utalii, biashara na ajira kwa wananchi wa nchi hizo tatu.

Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Makonda amesema fedha hizo zinatarajiwa kuzunguka katika sekta mbalimbali, ikiwemo hoteli, usafiri, huduma za chakula, matangazo na biashara ndogondogo.

“AFCON 2027 si mashindano ya soka pekee, bali ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa Watanzania. Tunatarajia mzunguko wa fedha unaokadiriwa kufikia dola bilioni mbili, hivyo ni muhimu wafanyabiashara kujiandaa mapema, kuboresha huduma zao na kutumia mifumo ya kidijitali ili kunufaika na fursa zitakazotokana na mashindano haya,”amesema .

Amesema mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani, huku takribani watu bilioni tatu wakitarajiwa kufuatilia kupitia televisheni, jambo litakalotoa nafasi ya kuitangaza Tanzania kimataifa.

Makonda amesema Tanzania itakuwa mwenyeji wa baadhi ya mechi katika miji ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar, hivyo akazitaka sekta zinazohusika na wafanyabiashara kujiandaa mapema ili kunufaika na wageni watakaofika nchini.

Amesema changamoto haitakuwa kukosekana kwa soko, bali uwezo wa wafanyabiashara kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wageni. Amewahimiza kuboresha biashara zao, kuongeza uwezo wa uzalishaji na kutumia mifumo ya kidijitali kujitangaza na kuwafikia wateja.

Amesema kuwa mafanikio ya AFCON 2027 hayapaswi kupimwa kwa ubora wa michezo pekee, bali pia kwa ajira zitakazozalishwa, biashara zitakazokua, ongezeko la watalii na manufaa yatakayobaki kwa wananchi baada ya mashindano kumalizika.

Makonda amesema Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira ya usalama na huduma muhimu yanakuwepo ili timu, wageni na mashabiki watakaofika nchini wapate huduma bora.

Amesema ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda pia ni fursa ya kuimarisha umoja wa Afrika Mashariki na kuitangaza kanda hiyo kwa pamoja.

Akizungumzia lugha ya Kiswahili, Makonda amehimiza nchi hizo tatu kuendelea kuitumia na kuipa nafasi katika shughuli za kimataifa za michezo, akisema ni lugha inayounganisha watu wa mataifa mbalimbali na kuimarisha mshikamano wa Afrika Mashariki.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Tanzania, Kenya na Uganda kwa mchango wao katika kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo, akisema AFCON 2027 inapaswa kuwa urithi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa nchi hizo.

Related Articles

Back to top button