Ligi Kuu

Barker: Tunataka ubingwa wa Afrika

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema wanahitaji kuanza kwa ushindi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapokutana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini Jumapili, Novemba 29, akisisitiza kuwa mwanzo mzuri ni muhimu katika safari ya kutafuta ubingwa wa mashindano hayo.

Barker amesema lengo la Simba ni kutwaa ubingwa wa Afrika, lakini wanatambua kuwa mafanikio hayo yanahitaji kupita hatua mbalimbali, kuanzia hatua ya makundi kabla ya kuelekea mechi za mtoano.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, kocha huyo amesema Simba inapaswa kutumia vizuri nafasi ya kucheza nyumbani kwa kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika mchezo wake wa kwanza wa kundi.

Amesema uzoefu wa msimu uliopita, ambao Simba ilipoteza michezo yake mitatu ya mwanzo katika hatua ya makundi, ni funzo muhimu linalopaswa kuwafanya wawe makini zaidi safari hii.

“Tunataka kushinda Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo kwa timu nyingine 16 zinazoshiriki. Lakini ili kufikia lengo hilo, lazima tupitie hatua mbalimbali. Kwanza tunahitaji kufanya vizuri katika hatua ya makundi na kuhakikisha tunamaliza katika nafasi zinazotuwezesha kufuzu hatua ya mtoano,” amesema Barker.

Ameongeza: “Ni muhimu kuanza vizuri. Huu ni mchezo wetu wa nyumbani na tunapaswa kuhakikisha hatuanzi vibaya kama msimu uliopita ambapo klabu ilipoteza michezo yake mitatu ya kwanza. Ikifika hatua hiyo inakuwa vigumu kurejea.”

Kuhusu kuifahamu Orlando Pirates, Barker amesema anaifahamu timu hiyo kutokana na kukutana nayo mara kadhaa akiwa kocha wa Stellenbosch, huku pia akiwa na uzoefu wa kumfahamu kocha wake.

Hata hivyo, amesema uzoefu huo hauwezi kuwa dhamana ya ushindi, hivyo wachezaji wake wanapaswa kutekeleza kikamilifu mpango wa mchezo ili kupata matokeo wanayoyahitaji.

Related Articles

Back to top button