Mastaa

Ndoa ya siri ya Miley Cyrus, Maxx Morando bado gumzo

CALIFORNIA: NDOA ya mwanamuziki maarufu wa Marekani, Miley Cyrus, na mpenzi wake wa muda mrefu, Maxx Morando, imeendelea kuwa gumzo licha ya kufanyika kwa siri huko mjini Palm Springs, California, Marekani.

Ndoa hiyo iliyofungwa, Novemba 21, 2026 imewekwa wazi na Cyrus, mwenye umri wa miaka 33 kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kuchapisha picha za harusi yao zikiwa na ujumbe mfupi wa herufi ‘M + M’ pamoja na tarehe 21.11.26. Picha hizo zilimuonesha akiwa na mumewe katika mavazi ya harusi huku wakikumbatiana na kubusiana baada ya kufunga ndoa.

Katika sherehe hiyo, mwimbaji huyo alivaa gauni jeupe la hariri lenye mikono mirefu lililotengenezwa na kampuni ya mitindo ya Saint Laurent, huku Morando, mwenye umri wa miaka 28, akivalia suti nyeusi. Harusi hiyo ilifanyika katika mazingira ya faragha, ikihusisha watu wa karibu na familia zao.

Baadhi ya wanafamilia waliohudhuria ni pamoja na mama yake Miley, Tish Cyrus, baba yake Billy Ray Cyrus na dada yake Noah Cyrus. Kwa mujibu wa jarida la People, familia ya mwimbaji huyo ilitaka siku hiyo iwe ya kipekee na yenye furaha kwake.

Miley na Morando walianza kuhusishwa kimapenzi mwaka 2021 baada ya kutambulishwa kupitia miadi ya kimapenzi iliyopangwa na watu wengine. Cyrus aliwahi kueleza katika mahojiano na jarida la British Vogue mwaka 2023 kuwa walikutana kupitia utaratibu huo wa kufahamiana kabla ya uhusiano wao kuendelea.

Uhusiano wao uliendelea kwa miaka kadhaa kabla ya kufikia hatua ya uchumba. Cyrus alithibitisha kuwa amechumbiwa na Morando mwaka 2025, huku mwanamuziki huyo akieleza kuwa alimposa wakati walipokuwa safarini nchini Japan, katika jiji la Kyoto.
Morando ni mpiga ngoma, mtunzi na mtayarishaji wa muziki ambaye ni sehemu ya kundi la muziki wa rock la Liily, lenye makazi yake Los Angeles. Kabla ya ndoa hiyo, wawili hao pia walikuwa wakishirikiana katika shughuli za muziki, hatua iliyozidi kuimarisha uhusiano wao wa kimapenzi na kisanii.

Kwa Miley Cyrus, ndoa hiyo ni ukurasa mpya wa maisha yake ya kimapenzi baada ya ndoa yake ya awali na mwigizaji Liam Hemsworth, ambayo ilifungwa mwaka 2018 na kuvunjika mwaka 2020. Ndoa yake na Morando imepokelewa kwa pongezi kutoka kwa mashabiki mbalimbali duniani kupitia mitandao ya kijamii.

Related Articles

Back to top button