Azam yaanza kutangaza vifaa vipya

KLABU ya Azam imeanza kujiwinda kwa msimu mpya 2024/2025 kwa kuanza kutangaza wachezaji wapya iliyowasajili.
Kupitia mitandao yake rasmi ya kijamii imetangaza kumsajili mshambuliaji kutoka Colombia, Jhonier Blanco.
“Tunayo furaha kutangaza kwamba tumekamilisha uhamisho wa mshambuliaji raia wa Colombia, Jhonier Blanco, kutoka klabu ya Aguilas Doradas ya mji wa Rionegro, inayoshiriki Ligi Kuu ya Colombia,” imesema Azam kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Azam imesema Blanco aliyezaliwa Oktoba 18, 2000, amesaini mkataba wa miaka minne baada ya kufaulu vipimo vya afya, kufuatuatia makubaliano baina ya klabu yake na Azam.
Kwa mujibu wa washindi hao wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara alianzia soka lake kwenye akademi ya Club Deportivo Estudiantil kabla ya kujiunga na timu ya ligi kuu ya Aguilas Doradas.
Taarifa hiyo ya Azam imesema Blanco alitolewa kwa mkopo kwenye klabu ya daraja la kwanza ya Fortaleza. Akiwa na klabu hiyo, akaibuka kuwa mfungaji bora akiisaidia kupanda daraja.
Baada ya mkopo akarudi klabuni kwake Aguilas Doradas hadi sasa ambapo Azam imemnunua.