Zaidi ya watu 12,000 waokolewa katika tamasha la Don Toliver

MANCHESTER: ZAIDI ya watu 12,000 wameondolewa kwa dharura katika ukumbi wa Co-op Live mjini Manchester, Uingereza, baada ya dutu isiyojulikana kusambaa katikati ya mashabiki wakati wa onesho la mwanamuziki wa Marekani, Don Toliver.
Tukio hilo lilitokea, wakati msanii huyo alipokuwa akitumbuiza katika ukumbi huo, ambapo baadhi ya mashabiki walianza kukohoa, kushindwa kupumua vizuri na kupata muwasho machoni baada ya kunusa harufu kali iliyosambaa ndani ya ukumbi.
Kwa mujibu wa polisi wa Greater Manchester, tukio hilo liliripotiwa majira ya saa nne usiku, hali iliyosababisha kutangazwa kwa tukio kubwa la dharura ili kuratibu shughuli za uokoaji na kuhakikisha usalama wa watu wote waliokuwapo ukumbini hapo.
Huduma za ambulansi za eneo la Kaskazini Magharibi mwa Uingereza ziliripoti kuwa zaidi ya watu 80 walifanyiwa uchunguzi wa afya kutokana na matatizo ya macho na mfumo wa upumuaji, huku mtu mmoja akipelekwa katika Hospitali ya Manchester Royal Infirmary kwa matibabu zaidi.
Awali kulikuwa na taarifa kuwa huenda dutu hiyo ilikuwa gesi ya kutoa machozi, lakini polisi walisema bado wanaendelea na uchunguzi kubaini aina ya dutu iliyosambazwa na chanzo chake. Uongozi wa ukumbi wa Co-op Live ulisema unashirikiana na polisi katika uchunguzi wa tukio hilo.
Kutokana na tukio hilo, onesho la Don Toliver lililokuwa limepangwa kufanyika katika ukumbi wa O2 jijini London Jumatatu, Novemba 23, liliahirishwa hadi Desemba 15, 2026. Msanii huyo alieleza kuwa usalama wa mashabiki wake ni muhimu na alitaka kuhakikisha onesho linalofuata linafanyika katika mazingira salama.




