Ligi Daraja La Kwanza

KMC yaporomoka, Mtibwa yaongoza Championship

DAR ES SALAAM: KMC imejikuta ikishuka kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi ya Championship baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Tanzania Prisons kwa bao 1-0, matokeo yaliyobadilisha mpangilio wa timu tatu za juu katika ligi hiyo.

Mabadiliko hayo yametokea baada ya michezo ya raundi ya 10, ambapo Mtibwa Sugar imepanda hadi kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 21 baada ya kuichapa Songea United mabao 3-1.

Ushindi huo umeiwezesha Mtibwa kuipiku KMC iliyokuwa ikiongoza ligi hiyo kwa muda, huku Tanzania Prisons nayo ikipanda hadi nafasi ya pili kwa pointi 20 baada ya kuifunga KMC na kuifikisha pointi 19.

Kwa upande wa KMC, kushuka hadi nafasi ya tatu ni pigo katika mbio zake za kurejea kileleni, hasa ikizingatiwa kuwa ilikuwa na nafasi nzuri ya kuendelea kuongoza ligi hiyo. Kupoteza pointi tatu dhidi ya Prisons kumeipa nafasi Mtibwa na wapinzani wengine kubadili mwelekeo wa ushindani.

Hata hivyo, tofauti ya pointi mbili kati ya Mtibwa inayoongoza na KMC iliyo nafasi ya tatu inaonesha kuwa ushindani bado ni mkali na nafasi za juu zinaweza kubadilika tena katika michezo ijayo.

Related Articles

Back to top button