Afrika Mashariki

Tiketi 15,000 za mechi ya Bayern na Ajax itakayopigwa Kenya zimeuzwa zote

NAIROBI, Kenya: HAMASA ya mashabiki wa soka nchini Kenya imeonekana wazi baada ya tiketi zote 15,000 zilizotolewa katika awamu ya kwanza kwa ajili ya mchezo wa kirafiki kati ya Bayern Munich ya Ujerumani na Ajax Amsterdam ya Uholanzi kuuzwa ndani ya muda mfupi.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Januari 5, 2027, katika Uwanja wa Raila Odinga International Stadium uliopo Talanta Sports City, jijini Nairobi, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa uwanja huo mpya wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000.

Kwa mujibu wa taarifa za waandaaji, mauzo ya tiketi yalifunguliwa Novemba 5, huku awamu ya kwanza ikimalizika Novemba 10.

Bei za tiketi katika awamu hiyo zilianzia shilingi za Kenya 2,500 sawa na shilingi za Tanzania 51,125, Shilingi za Kenya 3,500 sawa na TSh 71,575 na Ksh 5,000 sawa na TSh 102,250 kwa maeneo ya kawaida.

Bei nyingien za tiketi zilikuwa zikiuzwa kwa KSh 15,000 sawa na TSh 306,750 na KSh 20,000 sawa na TSh 409,000.
Makundi ya bei nafuu yalipata uhitaji mkubwa na kuuzwa ndani ya saa chache baada ya mfumo wa mauzo kufunguliwa.

Hata hivyo, waandaaji wamewahakikishia mashabiki ambao hawakufanikiwa kupata tiketi kuwa kutakuwa na awamu nyingine za mauzo. Hivyo, kuisha kwa tiketi 15,000 hakumaanishi kuwa tiketi zote za mchezo huo zimekwisha, bali ni mgao wa awamu ya kwanza pekee.

Kwa upande wa maandalizi, mchezo huo una umuhimu mkubwa kwa Kenya kwani utakuwa kipimo cha uwezo wa nchi kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa kabla ya michuano ya AFCON 2027, ambayo Tanzania itaandaa kwa Pamoja na Kenya na Uganda.

Waandaaji wanatarajia kutumia tukio hilo kupima mifumo ya usalama, usafiri, udhibiti wa umati, huduma za mashabiki na uendeshaji wa uwanja.

Aidha, mchezo huo unatarajiwa kuwakutanisha klabu mbili zenye historia kubwa barani Ulaya, huku mamlaka za michezo nchini Kenya zikisema timu hizo zimeahidi kuleta vikosi vyao imara vya wachezaji wa kikosi cha kwanza. Hata hivyo, orodha ya mwisho ya wachezaji watakaosafiri Nairobi bado haijathibitishwa rasmi.

Related Articles

Back to top button