Eric Omondi akusanya milioni 114.5 kwa saa 48

KAKAMEGA, Kenya: MCHEKESHAJI na mwanaharakati Eric Omondi ametangaza kufanikiwa kukusanya jumla ya shilingi za Kenya 5,665,000 sawa na zaidia ya milioni 114 ndani ya saa 48 kupitia kampeni ya kuchangisha fedha ya ‘Sisi Kwa Sisi’.
Omondi alichangisha fedha hizo kwa ajili ya kumsaidia kijana Bryson Makokha kutoka Kakamega anayesumbuliwa na ugonjwa wa ngozi.
Baada ya kusambaa kwa video inayomuonesha Bryson akiuza ndizi mitaani ili kujipatia kipato, Eric aliamua kuingilia kati na kutoa msaada kwa kijana huyo pamoja na familia yake. Bryson amesafirishwa hadi Nairobi kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini tatizo lake la kiafya.
Akizungumza kuhusu hatua inayofuata, Eric aliweka wazi mipango minne ya kumsaidia Bryson na familia yake, ikiwemo kugharamia matibabu yake, kujenga nyumba mpya kwa ajili ya wazazi wake, kumlipia karo ili aweze kurejea shuleni na kuanzisha biashara ya duka la rejareja litakalouza bidhaa kama mkate, maziwa, mboga na matunda.
Changamoto ya Bryson imekuwa ikimkabili kwa takribani miaka minane, huku akieleza kuwa ugonjwa huo alikuwa nao tangu kuzaliwa. Alisema amekuwa akipata nafuu anapotumia dawa, lakini dalili hurudi tena mara tu dawa zinapoisha, licha ya kutembelea vituo mbalimbali vya afya.
Hali yake ya kiafya imekuwa ikiathiri pia uwezo wake wa kufanya biashara, kwani alikuwa akiuza ndizi moja kwa shilingi tano za Kenya, lakini baadhi ya wateja walikuwa wakisita kununua kutokana na hali ya ngozi yake. Kwa upande mwingine, mama yake pia ana matatizo ya kiafya yanayohitaji upasuaji wa tumbo.
Eric amewashukuru Wakenya waliojitokeza kuchangia kupitia kampeni hiyo, akisisitiza kuwa fedha zilizokusanywa zitasaidia kubadilisha maisha ya Bryson na familia yake kwa kuwapatia matibabu, makazi bora na fursa ya kujikwamua kiuchumi.




