Muziki

Summerellah atoa onyo rushwa ya ngono katika mziki

DAR ES SALAAM: MSANII chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva, Nasra Abubakar maarufu kama Summerellah, ambaye ni mshindi wa nafasi ya tatu katika shindano la Bongo Star Search (BSS) 2026, ametoa wito kwa wasanii wa kike kujiamini na kutumia vipaji vyao kujijengea nafasi katika tasnia ya muziki badala ya kutegemea mahusiano ya kimapenzi kupata mafanikio.

Summerellah, aliyetokea Dodoma, amesema anaamini katika uwezo na kipaji chake, akisisitiza kuwa safari ya mafanikio katika muziki inapaswa kujengwa kupitia ubunifu, juhudi na nidhamu ya kazi.

Akizungumza na SpotiLeo, msanii huyo amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia ukaribu wa kimapenzi na watu wenye ushawishi kama njia ya kupata nafasi katika tasnia ya muziki, jambo ambalo amesema linaweza kuwazuia wasanii kujenga misingi imara ya kisanaa.

Amesema wasanii wa kike wanapaswa kujitambua, kuthamini vipaji vyao na kutokubali mazingira yanayoweza kuwafanya watumie mahusiano badala ya uwezo wao kupata fursa za kimuziki.

“Wasanii wanapaswa kujiamini na kuweka nguvu katika kazi zao badala ya kutegemea mahusiano ili kupata nafasi. Ni muhimu kujenga jina kupitia kipaji na kazi nzuri kwa sababu ndiyo inayoweza kuwapa msingi imara na wa kudumu katika muziki,” amesema.

Aidha, Summerellah ametoa wito kwa washereheshaji wa sherehe na matukio mbalimbali kuheshimu ratiba za wasanii wanapoalikwa kutumbuiza, akieleza kuwa kuzingatia muda waliopangiwa ni sehemu ya kuthamini kazi zao.

Amesema wasanii wanahitaji kupewa nafasi na mazingira mazuri ya kutumbuiza ili waweze kuwasilisha kazi zao ipasavyo na kuwafurahisha mashabiki wanaohudhuria matukio hayo.

Ameongeza kuwa muziki ni kazi inayohitaji heshima na kuthaminiwa, hivyo waandaaji wa matukio wanapaswa kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri unaowawezesha wasanii kutekeleza majukumu yao bila changamoto za ratiba.

Kwa upande wake, Summerellah anaeleza kuwa ana malengo makubwa katika safari yake ya muziki na anatarajia kutumia kipaji chake, nidhamu na ubunifu kujenga nafasi katika soko la Bongo Fleva.

Nafasi yake ya tatu katika Bongo Star Search 2026 imekuwa hatua muhimu katika safari yake ya kisanaa, huku akielekeza nguvu katika kujijenga kama msanii anayetarajia kushindana katika soko la muziki nchini.

Related Articles

Back to top button