Marekani yajiondoa Kombe la Dunia U17 Qatar kwa hofu za kiusalama

NEW YORK: MAREKANI imejiondoa katika michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U17), inayotarajiwa kuanza Novemba 19 nchini Qatar, kutokana na hofu za kiusalama katika eneo la Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani.
Kwa mujibu wa US Soccer Collective na The Athletic, wakinukuu vyanzo visivyotajwa majina, wachezaji wa kikosi hicho walifahamishwa kuhusu uamuzi huo zaidi ya wiki moja kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Marekani (US Soccer) halikuwa limethibitisha rasmi taarifa hizo wala kujibu ombi la AFP la kutoa ufafanuzi.
Mvutano wa Mashariki ya Kati umeongezeka tangu kuanza kwa vita mwezi Februari kufuatia mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ambayo nayo yalijibu kwa kushambulia maeneo mbalimbali, yakiwemo mataifa ya Ghuba yanayoshirikiana na Washington.
Jitihada za kidiplomasia za kumaliza vita hivyo zimekuwa zikikumbwa na vitisho vya mara kwa mara kutoka Marekani na Israel kuhusu uwezekano wa kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran.
Hali hiyo imeathiri pia ratiba za mashindano mbalimbali ya michezo katika eneo hilo.
Fainali za tenisi za WTA zilizokuwa zimepangwa kufanyika Saudi Arabia zimehamishiwa Indian Wells nchini Marekani. Aidha, mashindano ya magari ya Formula One (F1) nchini Saudi Arabia yalifutwa, huku mashindano yaliyokuwa yafanyike Bahrain yakisitishwa na baadaye kupangwa upya kufanyika Malaysia.
Matukio kadhaa ya michezo nchini Saudi Arabia pia yamefutwa au kuahirishwa katika wiki za hivi karibuni kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na waasi wa Houthi kutoka Yemen.
Marekani ilikuwa miongoni mwa mataifa 48 yaliyopangwa kushiriki Kombe la Dunia U17 nchini Qatar, ambapo ilipangwa kuwa katika kundi moja na Montenegro, Chile na Algeria.
Mashindano hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka tangu mwaka jana na Qatar imepewa jukumu la kuwa mwenyeji kwa miaka mitano mfululizo.
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilipotangaza Qatar kuwa mwenyeji mwaka 2024, lilisema uamuzi huo ulilenga kutumia miundombinu ya soka iliyopo nchini humo ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha uendelevu wa mashindano.
Qatar pia ilikuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la wanaume mwaka 2022.




