Muziki

Brandy, Monica kufanya tamasha la Pamoja Las Vegas 2027

MASTAA wa muziki wa R&B, Brandy na Monica, wametangaza kufanya tamasha lao la kwanza la pamoja jijini Las Vegas, Marekani, lililopewa jina la ‘The Boy Is Mine Vegas Residency’, kufuatia mafanikio ya ziara zao za pamoja za muziki.

Wasanii hao walitangaza habari hiyo wakati wa kipindi cha televisheni cha Dancing with the Stars, muda mfupi baada ya kutoa burudani kwa kuimba wimbo wao maarufu The Boy Is Mine uliotamba mwaka 1998.

Tamasha hilo litakalosimamiwa na kampuni ya Black Promoters Collective litakuwa na maonesho 10 maalumu katika ukumbi wa Resorts World Las Vegas. Linatarajiwa kuanza Mei 29, 2027 na kuhitimishwa Julai 17, mwaka huo huo.

Akizungumzia ushirikiano wao, Monica alisema awali walipanga kufanya ziara moja tu ya pamoja, lakini baada ya maonesho ya kwanza aligundua kuwa walikuwa na uhusiano mkubwa zaidi wa kimuziki na kibinafsi. Alisisitiza kuwa mawasiliano ndiyo msingi muhimu unaoimarisha ushirikiano wao.

Mashabiki wanatarajiwa kupata burudani inayochanganya nyimbo zao binafsi na zile walizofanya kwa pamoja. Brandy anatarajiwa kuimba vibao kama Full Moon na Angel of Mine, huku Monica akitarajiwa kuwakumbusha mashabiki nyimbo zake maarufu zikiwemo The First Night na So Gone.

Brandy na Monica, ambao wote ni washindi wa tuzo za Grammy, walijulikana sana katika miaka ya 1990 kutokana na ushindani wao wa kimuziki, lakini sasa wameunganisha nguvu na kuendeleza urafiki wao kupitia muziki. Tamasha hilo linatarajiwa kurejesha kumbukumbu za enzi za dhahabu za R&B za miaka ya 1990 na 2000.

Related Articles

Back to top button