Masumbwi

Deboura: Ushindi lazima

DAR ES SALAAM: “Ushindi ni lazima, sitaki ushindi wa majaji, nataka ushindi ulingoni,” hiyo ni kauli ya bondia mrembo Debora Mwenda kuelekea pambano lake dhidi ya Fatuma Mustapha Desemba 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Debora amesema amejipanga kuhakikisha anamaliza mwaka kwa ushindi katika pambano hilo la Usiku wa Mabingwa, litakalofanyika siku ya Boxing Day, akisisitiza kuwa mpinzani wake anatakiwa kujiandaa kukabiliana na mabadiliko makubwa aliyoyafanya.

“Huruma si malezi, mpinzani wangu ajiandae kwa sababu nimebadilika. Nawakaribisha wapenzi wa ngumi na mashabiki wangu kuja kushuhudia pambano langu la kufungia mwaka. Itakuwa pambano zuri,” amesema Debora.

Bondia huyo amesema katika maandalizi yake ameboresha mfumo wa mapambano kwa kuongeza mashambulizi ya mwili, hasa maeneo ya tumbo na mbavu, akiamini mbinu hizo zitampa nafasi ya kumuweka mpinzani wake katika wakati mgumu.

Kwa upande wake, Adam Nazaro maarufu Jaguar, nahodha wa Debora, amesema bondia huyo amefanyiwa maboresho makubwa na mpinzani wake hatakiwi kudhani atakutana na Debora wa zamani.

Jaguar amesema nguvu na uwezo wa Debora katika kutumia mashambulizi ya mwili ni miongoni mwa mambo ambayo mpinzani wake anapaswa kujiandaa kukabiliana nayo.

Naye kocha wa bondia huyo, Mohammed Yusufu, amesema maandalizi yanaendelea vizuri na kwamba Debora amebadilika katika mbinu na mfumo wa mapambano, hivyo mpinzani wake anapaswa kujiandaa kwa kazi ngumu.

Amesema muonekano wa Debora nje ya ulingo usimfanye mpinzani wake kumchukulia kirahisi, kwani anapoingia ulingoni hubadilika na kuwa mpambanaji mwenye dhamira ya kupata ushindi.

Yusufu amesema wamejipanga kupambana bila kumhurumia mpinzani, akisisitiza kuwa kazi iliyofanyika wakati wa maandalizi itaonekana ulingoni.

Related Articles

Back to top button