BASATA yawafutia usajili MC Mtoto wa Mama na Mzee wa Ngenga

DAR ES SALAAM: Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limefuta usajili wa wasanii wawili, Dannyel Claud John maarufu kama MC Mtoto wa Mama na Hassan Ally Matupa anayefahamika kwa jina la Mzee wa Ngenga, kuanzia Novemba 5, 2026.
Uamuzi huo umetokana na kile ambacho BASATA imebaini kuwa ni ukiukwaji wa Kanuni ya 20 (2) (j) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la Mei 22, 2026.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo, msanii anatakiwa kuhakikisha kuwa kazi anazowasilisha kwa umma hazina maudhui yanayoshawishi au kuhamasisha vitendo vya ngono, ushoga, usagaji, ulawiti, unajisi wa watoto pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.
BASATA imeeleza kuwa wasanii hao walikiuka masharti hayo licha ya kufahamu wajibu wao wa kuendesha shughuli za sanaa kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo nchini.
Katika hatua nyingine, BASATA imeonya kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 32 (b) na (c), mtu au mdau yeyote wa sanaa haruhusiwi kuwashirikisha au kuwatumia wasanii hao katika shughuli zozote za sanaa.
Baraza hilo limefafanua kuwa mtu yeyote atakayekiuka agizo hilo atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa kanuni husika.
Hata hivyo, MC Mtoto wa Mama na Mzee wa Ngenga bado wanaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya sanaa ndani ya siku 30.
Hatua hiyo imeibua mjadala katika tasnia ya burudani nchini kuhusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na maadili katika kazi zinazowasilishwa kwa umma.




