Serengeti Boys mawazo yote Kombe la Dunia

DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya Wavulana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, imeondoka leo kuelekea Qatar kwa ajili ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza Novemba 19 hadi Desemba 13, mwaka huu nchini Qatar.
Tanzania inakwenda kushiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo, ikiwa ni hatua kubwa kwa maendeleo ya soka la vijana nchini baada ya mafanikio ya kikosi hicho katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zilizofanyika Morocco mwaka huu.
Katika fainali hizo, Serengeti Boys ilifanikiwa kufika hatua ya mwisho na kupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika jukwaa kubwa la soka la vijana duniani.
Tanzania imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Ireland na Costa Rica, ambapo itaanza kampeni yake Novemba 21 kwa kucheza na Costa Rica kabla ya kukutana na Brazil Novemba 24 na kumalizia hatua ya makundi dhidi ya Ireland Novemba 27.
Katika maandalizi yake kuelekea mashindano hayo, Serengeti Boys pia imepata nafasi ya kucheza mechi nyingi za kirafiki za kimataifa nchini Korea Kusini na Azerbaijan hivi karibuni katika kujiweka imara na tayari kwa michuano hiyo mikubwa.




