Nyumbani

Mtambo wa mashuti watua Msimbazi

DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba imeendelea kufanya maboresho ya kikosi cha timu hiyo kwa kumtambulisha rasmi mshambuliaji Steven Mukwala raia wa Uganda kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Asante Kotoko ya Ghana.

Usajili huo wa mshambuliaji unatarajiwa kuongeza uimara wa kikosi hicho kwenye safu ya ushambuliaji akisaidiana na Fred Michael aliyejiunga na timu hiyo kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Akizungumza na Spotileo, Meneja wa Idara ya habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema moja ya maeneo lilikuwa na mapungufu msimu uliopita ni safu ya ushambuliaji.

Amesema ujio wa mshambuliaji huyo utaongeza uimara katika safu hiyo kwa kusaidia na washambuliaji waliopo ndani ya timu hiyo kwa msimu ujao wa mashindano.

“Tumeweza kupata dawa ya safu yetu ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita haikuwa imara, sasa tunaendelea kushusha vifaa, Mukwala ni mtu na tumeridhishwa na uwezo wake”.

“Usajili tunaoufanya ni kuvunja na kununua mikataba ya wachezaji huko walikotoka, hilo linaendelea, baada ya Mukwala kila siku tutatambulisha mchezaji hadi tutakapomaliza usajili wetu,” amesema Ahmed.

Ahmed amewataka mashabiki kuwa watulivu na kuongeza kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ni kinara mwenye uwezo wa kufunga na wanategemea atakuwa msaada mkubwa kwenye timu hiyo.

Mshambuliaji huyo amefunga mabao 14 na kusaidia kupatikana kwa mengine mawili katika Michezo 28 katika ligi kuu Ghana, amewahi kuzitumikia klabu ya Vipers, Maroons FC zote za Uganda kabla ya kutimkia Ghana kucheza Asante Kotoko.

Related Articles

Back to top button