Muziki

Malaika Gray atikisa Apple Music

'My fever’ yaingia playlist tisa

DAR ES SALAAM: Msanii na mwimbaji anayechipukia katika muziki wa Bongo Fleva, Malaika Gray, ameanza rasmi safari yake ya muziki kwa mafanikio baada ya wimbo wake wa kwanza, My Fever, aliomshirikisha Marioo, kuingia katika playlist tisa za Apple Music ndani ya wiki moja tangu kuachiwa kwake.

Miongoni mwa playlist hizo ni Africa Now, inayokusanya nyimbo 100 kutoka maeneo mbalimbali barani Afrika. Kwa sasa, My Fever imefikia nafasi ya 54 katika playlist hiyo.

Katika playlist ya Africa Now, Malaika Gray na Marioo ni miongoni mwa wasanii waliojumuishwa pamoja na msanii wa Uganda, Joshua Baraka, kupitia wimbo wake Commando aliomshirikisha Tiwa Savage.

Mbali na Africa Now, wimbo huo umefanikiwa kuingia katika playlist nyingine nane za Apple Music ambazo ni New Music Daily, Afro Soul Mix, Alpha Women, Viral Afrobeats, Motherland Honey, Africa Rising, New in Afrobeats na East Africa Wave, na kufanya jumla ya playlist alizofikia kuwa tisa.

Hatua hiyo inaipa My Fever nafasi ya kuwafikia wasikilizaji wengi zaidi katika masoko tofauti ya muziki, huku ikimfungulia Malaika Gray milango ya kujitambulisha kama msanii mwenye kazi rasmi ndani na nje ya Tanzania.

Mafanikio hayo yanaenda sambamba na mwitikio wa video ya wimbo huo, ambayo imevuka watazamaji 900,000 kwenye YouTube ndani ya siku tano pekee tangu ilipotoka.

Wimbo My Fever umetayarishwa na mtayarishaji wa muziki Abbah na kumkutanisha Malaika Gray na Marioo katika ushirikiano unaokuja kuwa sehemu muhimu ya mwanzo wa safari yake ya muziki.

Kabla ya kuanza kutoa kazi zake rasmi, Malaika Gray alikuwa akijenga utambulisho wake kwa kuimba cover za nyimbo mbalimbali, jambo lililomsaidia kuwafikia na kuwavutia baadhi ya wapenzi wa muziki.

Kupitia My Fever, sasa anaanza ukurasa mpya wa safari yake ya kisanii, huku mafanikio ya awali kwenye majukwaa ya muziki na YouTube yakimpa nafasi ya kutambulisha kipaji chake kwa hadhira pana zaidi.

Je, huu ni mwanzo wa jina jipya kubwa katika muziki wa Bongo Fleva?

Related Articles

Back to top button