Ligi Kuu

Mangungu: Maslahi binafsi yanachafua Simba

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Simba Sports Club, Murtaza Mangungu, amedai kuwa baadhi ya watu wanaohusika na masuala ya klabu hiyo wanaweka mbele maslahi yao binafsi badala ya ustawi wa Simba, akitaka taratibu za umiliki na uendeshaji zifuatwe kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi.

Mangungu amesema wanachama waliowapa dhamana ya kuwakilisha maslahi yao wanapaswa kulindwa kwa kuhakikisha maamuzi yanayofanywa ndani ya klabu yanazingatia katiba na taratibu zilizowekwa, badala ya kuongozwa na maslahi ya watu binafsi.

Akizungumzia suala la kampuni ya Simba Sports Club Company Limited, amesema katiba ya klabu inaeleza majukumu ya kampuni hiyo katika kusimamia shughuli za kibiashara na kiutendaji, huku umiliki wa hisa ukihusisha Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama pamoja na wawekezaji kwa mujibu wa sheria.

Amesema mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu unapaswa kufuata masharti ya kisheria na kwamba ushiriki wa wawekezaji haupaswi kuwa sababu ya kupuuza taratibu zilizowekwa.

“Tunachotaka ni Simba iweze kwenda mbele kwa kufuata masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu,” amesema Mangungu.

Ameeleza kuwa mchakato wa kampuni hiyo ulihusisha taasisi mbalimbali, zikiwamo Tume ya Ushindani (FCC), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), lakini kwa maelezo yake, bado kuna masuala yanayohitaji ufafanuzi kuhusu ukamilifu wa mchakato huo.

Kuhusu mkutano mkuu, amesema taratibu za kuuitisha zinapaswa kufuata masharti ya katiba, akitaja Kifungu cha 21 kinachohusu mamlaka ya Mwenyekiti kuitisha mkutano kwa kushauriana na bodi. Ameeleza pia kuwa alipokea barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Michezo kuhusu mwongozo wa kuongeza muda wa kufanyika kwa mkutano mkuu.

Mangungu amesema siku ya kikao cha bodi hakuweza kuhudhuria kwa sababu alikuwa ameitwa TFF, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa katika kipindi hiki zinapaswa kuzingatia mwongozo wa mamlaka husika.

Aidha, amedai kuwa baadhi ya watu wanaweza kuwa na maslahi binafsi katika fedha zinazotumika kutokana na mgogoro huo, akionya kuwa matumizi hayo yanapaswa kuangaliwa kwa makini kwa kuwa yanaweza kuongeza gharama zinazohusishwa na deni la wawekezaji.

Related Articles

Back to top button